Tunakwenda kujifunza somo linaloitwa “MAANA YA NDOTO KIROHO”. Hapa tunakwenda kujifunza ndoto kwa uchambuzi wa kukidhi wenye utukufu wa Roho mtakatifu kitu wazungu wanaita ONEROLOGY na kama wengi wanavyodhani, hatutakwenda kufasiri ndoto wala kujifunza ufasiri wa ndoto  kitu wanaita ONEROCRITIC.

Marejeo Yetu:

Katika mafundisho yetu tutarejea sana katika kitabu kimoja tu BIBLIA na si vinginevyo / The only book to be our reference is Holy Bible.

SEHEMU YA KWANZA:

Katika sehemu ya kwanza ya somo letu tunakenda kuangalia mambo makuu mawili;

  • Ndoto ni nini?
  • Nini tofauti ya Ndoto na Maono?

Ndoto Ni Nini?

Katika Biblia yangu kuna neno NDOTO limeandikwa kama mara 68 hivi; kwenye Mwanzo pekee ipo mara 33 na kwenye kitabu cha Nabii Daniel mara 27 na kwa Agano Jipya naliona mara 8 pekee.

Wakati Biblia yangu imesheheni watumishi lukuki wa Mungu. Ni “watu wawili pekee” ndiyo ambao wametajwa katika “kufasiri NDOTO” ambao ni:

I. Yusufu na 

II. Daniel

Maana ya ndoto;

Ndoto; ni hali inayotokea kwa mtu wakati anapokuwa katika usingizi mzito; hiyo hali ni udhihirisho wa kama hayupo usingizini na anafanya mambo fulani ya kawaida (yaliyo dhahiri) ama mambo yasiyo ya kawaidi (yasiyo dhahiri).

Mambo dhahiri; Haya mambo ni kama kuota ndoto ambamo muna kama watu, wanyama waliopo duniano na vitu vya kawaida vilivyopo duniani.

Mambo yasiyo dhahiri; Haya ni mambo ya ajabu, mara nyingi hayapo katika ulimwengu wa kawaida. Unaota nyoka anabadili umbo anakuwa na umbo la mpira wa miguu, unaota wanyama wa kutisha sana, ama viumbe au vitu ambavyo havipo kabisa katika ulimwengu huu wa mwili na nyama.

Kwa mara ya kwanza kabisa NDOTO imeandikwa kwenye Biblia katika Mwanzo 20:3.

“Lakini Mungu akamjia Abimeleki katika ndoto ya usiku, akamwambia, Umekuwa mfu wewe kwa sababu ya mwanamke huyu uliyemtwaa, maana ni mkewe mtu.” Mwanzo 20:3

Walioota ndoto katika BIBLIA;

Wapo watu kadhaa katika Biblia wanatajwa kwamba waliota NDOTO. Tutawaona watu 10 katika Agano la Kale na watu 3 katika Agano Jipya na tutajifunza kidogo kuhusu NDOTO zao.

1. Mfalme ABIMELEKI wa Gerari (Misri):

Mungu alimjia Abimeleki katika NDOTO usiku, siku ambapo alilala na mke wa Ibrahim, Sara… Mungu akamjia mmataifa (Gentile) kwa ndoto kinyume cha kawaida, kwasababu ya mtu wake mpendwa Ibrahim.

“Lakini Mungu akamjia Abimeleki katika ndoto ya usiku, akamwambia, Umekuwa mfu wewe kwa sababu ya mwanamke huyu uliyemtwaa, maana ni mkewe mtu.” Mwanzo 20:3

2. YAKOBO mwana wa Isaka;

Yakobo aliota NDOTO yake akiwa ameondoka nyumbani, akafika sehemu iitwa Luzu ambapo yeye akapabatiza jina la BETHELI kwa maana ya kuamini kwamba ndipo penye lango la Mbinguni. Aliota ndoto ya KUBARIKIWA KWAKE.

“Akaota ndoto; na tazama, ngazi imesimamishwa juu ya nchi, na ncha yake yafika mbinguni. Tena, tazama, malaika wa Mungu wanapanda, na kushuka juu yake.” Mwanzo 28:12

Yakobo akaota NDOTO nyingine tena akiwa katika machungo ya mifugo wa mjomba wake Laban. Pale walipokubaliana na Laban kuhusu mshahara wa kuchunga… Bado Yakobo aliota ndoto ya BARAKA.

“Ikawa, wakati wale wanyama walipochukua mimba, naliinua macho yangu nikaona katika ndoto, na tazama, mabeberu waliowapanda hao wanyama walikuwa na milia, na madoadoa, na marakaraka.” Mwanzo 31:10

3. LABAN mjomba wa Yakobo, na mkwe.

Laban akiwa katika kumfuatia Yakobo baada ya kuondoka na miungu yake/vitu vya thamani na kwa kutoroka… Mungu alimjia huyu mtu wa mataifa tena kinyume na kawaida ila kwa manufaa ya mwanawe Yakobo. Alimwonya asije akamgusa Yakobo.

“Mungu akamjia Labani, Mshami, katika ndoto ya usiku, akamwambia, Ujihadhari, usimwambie Yakobo neno la heri wala la shari.” Mwanzo 31:24

4. YUSUFU mwana wa Yakobo;

Yusufu akiwa na nduguze 12 kwa baba yao Yakobo; aliota ndoto ya ukuu wake juu ya watu wa kwao ikiwa ni pamoja na Baba na mama. Aliota ukuu wake na Kubarikiwa kwake.

“Yusufu akaota ndoto, akawapa ndugu zake habari, nao wakazidi kumchukia;” Mwanzo 37:5

“Akaota tena ndoto nyingine, akawaambia ndugu zake, akasema, Angalieni, nimeota ndoto nyingine; na tazama, jua na mwezi na nyota kumi na moja zikaniinamia.” Mwanzo 37:9

5. MWOKAJI na MNYWESHAJI wa Ufalme wa Misri;

Hawa wawili wakiwa wamefungwa gereza moja pamoja na Yusufu; waliota ndoto katika usiku mmoja. Ni ndoto hizo ndizo zilizokusudiwa na Mungu kwaajili ya kumtoa kifungoni Yusufu na kuliinua jina lake.

“Wakaota ndoto wote wawili, kila mtu ndoto yake usiku mmoja, kila mtu kwa tafsiri ya ndoto yake, mnyweshaji na mwokaji wa mfalme wa Misri waliofungwa gerezani. Yusufu akawajia asubuhi, akawaona wamefadhaika.” Mwanzo 40:5-6

6. FARAO, Mfalme wa Misri:

Farao aliota ndoto, tena mara mbili katika usiku mmoja na akahitaji fasiri ya ndoto yake. Mungu alikusudia kumwotesha ndoto huyu mpagani kwaajili ya kuliinua jina la Yusufu na kutimiza ile ndoto ya Yusufu kuwa mkuu juu ya watu wa kwao.

“Ikawa, mwisho wa miaka miwili mizima, Farao akaota ndoto; na tazama, amesimama kando ya mto.” Mwanzo 41:1

“Akalala, akaota ndoto mara ya pili. Tazama, masuke saba yalimea katika bua moja, makubwa, mema.” Mwanzo 41:5

“Kisha hayo masuke membamba saba yakayala yale masuke saba makubwa yaliyojaa. Basi Farao akaamka, kumbe! Ni ndoto tu.” Mwanzo 41:7

7. MMIDIANI na mwenzake;

Mungu aliikusudia ndoto ile ambayo mmidiani aliiota na kufasiriwa na mwenzake tena kwa ufunuo wa Mungu; lengo lake ni kumjaza imani Gideon na jeshi lake dogo, hakika Gideon alijaa imani kama makusudi ya NDOTO.

“Hata Gideoni alipofika, tazama, palikuwa na mtu mmoja aliyekuwa akimhadithia mwenziwe ndoto, akasema, Tazama, naliota ndoto, na tazama, mkate wa shayiri ulianguka katika kambi ya Wamidiani, ukafika hata hema moja, ukaipiga hata ikaanguka, nao ukaipindua, hata ikalala chini. Mwenzake akamjibu akasema, Habari hii haikosi kuwa upanga wa Gideoni, mwana wa Yoashi, mtu wa Israeli. Mungu amewatia Wamidiani na jeshi lote katika mkono wake. Ikawa, aliposikia habari ya ile ndoto, na kufasiriwa kwake, akasujudu; akarudi katika jeshi la Israeli akasema, Inukeni, kwa maana Bwana amelitia jeshi la Midiani mikononi mwenu.” Waamuzi 7:13-15

8. Mfalme SULEMANI wa Israel;

Kwa hakika wapendwa tunafahamu sana kuwa Suleiman alikuwa Mfalme mwenye hekima sana na tajiri aliyebarikiwa mno… Na tunajua alipewa fursa (favor) na akaomba kupewa HEKIMA. Fursa alikuwa amepewa “kwa njia ya NDOTO.” Nachelea kusema wengi wetu tumepoteza baraka nyingi kwasababu ya kupuuza ndoto ama kukosa ujasiri katika ndoto.

“Na huko Gibeoni Bwana akamtokea Sulemani katika ndoto ya usiku; Mungu akamwambia, Omba utakalo nikupe.” 1 Wafalme 3:5

9. Mfalme NEBUKADREZA wa Babeli;

Mfalme huyu mpagani aliota ndoto na akataka fasiri bila kuwaambia ndoto, alisema ameisahau; alipoona hawajui akataka kuwachinja… Ndipo Daniel jina lake likasimama. Hapa utagundua kuwa pamoja na maana nyingine, ila Mungu alikusudia kumwinua mwanae kwa njia hiyo. Mfalme aliota kuhusu ile “sanamu kubwa ya dhahabu safi inayong’aa sana”.

“Mfalme akawaambia, Nimeota ndoto, na roho yangu imefadhaika hata niijue tafsiri yake.” Danieli 2:3

10. DANIEL aliyeitwa Belteshaza;

Daniel aliota ndoto muhimu sana katika utumishi wake. Ndiyo hii ndoto iliyomfanyabkuitwa kwa jina NABII. Alioota ndoto nayo akaiandika ndiyo inayoweka mlango wa saba wa kitabu chake. Ni ndoto ya ufunuo wa nyakati zilizopo kuendelea hadi zijazo.

“Katika mwaka wa kwanza wa Belshaza, mfalme wa Babeli, Danielii aliona ndoto, na maono ya kichwa chake, kitandani mwake; basi akaiandika ndoto, akatoa habari ya jumla ya mambo hayo.” Danieli 7:1

11. YUSUFU mume wa Maria;

Mungu alisema na Yusufu kwa njia ya NDOTO hata mara mbili. Alimwambia asimwache mchumba wake Maria kwaajili ya mimba. Na wakati mwingine akamwambia kuhusu kifo cha Herode na kwamba sasa warudi nyumbani kutoka uhamishoni.

“Basi alipokuwa akifikiri hayo, tazama, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akisema, Yusufu, mwana wa Daudi, usihofu kumchukua Mariamu mkeo, maana mimba yake ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu.” Mathayo 1:20

“Hata alipofariki Herode, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto huko Misri,” Mathayo 2:19

12. MAMAJUSI wa Mashariki;

Hawa walipokwenda kwenye ufalme wa Herode aliwaambia mkimwona mfamle ajaye mrudi kunipasha habari nikamsabahi nikampe nami zawadi. Lakini Mungu akasema na hawa mamajusi kwa njia ya NDOTO kuhusu dhamira ya Herodi na kwamba waondoke kwa kupitia njia nyingine.

“Nao wakiisha kuonywa na Mungu katika ndoto wasimrudie Herode, wakaenda zao kwao kwa njia nyingine.” Mathayo 2:12

“Na hao walipokwisha kwenda zao, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mama yake, ukimbilie Misri, ukae huko hata nikuambie; kwa maana Herode anataka kumtafuta mtoto amwangamize.” Mathayo 2:13

13. MKEWE Pilato;

Akiwa katika kutaka kutoa hukumu juu ya Yesu wa Nazareth, Pilato mkewe alimjia na kumuonya kutokunyoosha mkono wake juu ya Yesu kwasababu anakiri kupatabsana tabu usiku katika ndoto ya kwamba huyu Yesu kwamba ni mtu wa Haki na wala hana hatia. Nadhani utakumbuka ni Pilato ndiye aliyesema “mimi sioni hatia juu ya mtu huyu, nimenawa mikono yangu na damu yake isiwe juu yangu na nyumba yangu.”

“Na alipokuwa ameketi juu ya kiti cha hukumu, mkewe alimpelekea mjumbe, kumwambia, Usiwe na neno na yule mwenye haki; kwa sababu nimeteswa mengi leo katika ndoto kwa ajili yake.” Mathayo 27:19

Tofauti Ya Ndoto Na Maono:

Zipo namna tatu za kuingia katika ulimwengu wa ROHO. Namna hizo ni kwa NDOTO na MAONO na MAOMBI. Kwa maana hiyo NDOTO na MAONO zote ni njia za kuingia katika ulimwengu wa ROHO. Lakini pia NDOTO ni ufunuo wa picha na matukio; ilhali MAONO pia.

Tofauti yao inakuja kwamba MAONO humpata mtu akiwa macho kabisa, ubongo wake ukiwa active wakati NDOTO inamtokea mtu akiwa katika usingizi mzito sana, mwili umepumzika na ubongo unafanya kazi.

Ukisoma Biblia utakuta karibu maeneo yote; ndoto na maono yametumiwa kwa namna moja. Unaweza kukuta ndoto inaitwa maono ama maono yakaitwa ndoto. Lakini pia haijaathiri maana halisi ya tofauti zao.